Ijumaa 7 Novemba 2025 - 10:50
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Chile waungana na Palestina: Kukaa Kimya ni Sawa na Kushiriki Katika Uhalifu

Hawza/ Wanafunzi na wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Chile wamefanya hatua ya kisanii na ya upinzani katika Kitivo cha Falsafa na Sayansi ya Binadamu wakipinga uhalifu wa utawala wa Kizayuni na ukimya wa taasisi za elimu ya juu, huku wakidai kusitishwa kwa uhusiano wa kielimu na vyuo vya Kizayuni vya Israel.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, wakati taasisi nyingi za kielimu katika nchi za Magharibi zikinyamaza mbele ya janga la kibinadamu huko Ghaza, kundi la wanafunzi na wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Chile mnamo Jumatatu, tarehe 4 Oktoba, kutokana na ubunifu wa Kamati ya Palestina katika Chuo Kikuu cha Chile, waliandaa maonyesho ya sanaa ya upinzani katika eneo la Kitivo cha Falsafa na Sayansi za Binadamu, ili kufikisha sauti ya watu wa Palestina katika mazingira ya kitaaluma ya nchi hiyo.

Kwenye lango kuu la kitivo hicho, waliweka onyesho la picha lililojumuisha taswira za watoto wa Kipalestina waliouawa kishahidi, magofu ya Ghaza, na picha za wananchi wanaopinga uvamizi, kati ya picha hizo, kulikuwa na swali kubwa lililoandikwa kwa herufi pana ukutani:

“Mpaka lini vyuo vyetu vitakaa kimya mbele ya mauaji ya halaiki?”

Waandaaji wa tukio hilo walisema kuwa lengo lao kuu ni kuyavunja mazingira ya kutojali ndani ya vyuo vikuu na kutoa tahadhari dhidi ya hatari ya “kufanya uhalifu uonekane wa kawaida.” Walisema bayana kwamba kunyamaza mbele ya janga la kibinadamu huko Ghaza ni aina ya ushiriki katika uhalifu huo.

Katika taarifa rasmi ya Kamati ya Palestina, ilielezwa hivi: “Tangia Oktoba iliyopita, watu wa Palestina wamekuwa wakikabiliana na uvamizi usio na kifani — si tu kwa mabomu, bali kwa kuzingirwa, njaa na kufutwa utamaduni. Katika hali kama hii, kunyamaza na kutochukua hatua katika vyuo vikuu ni aina ya ushirikiano na dhulma.”

Wanafunzi katika taarifa hiyo walidai kuwa Chuo Kikuu cha Chile kifute mara moja mikataba yote ya ushirikiano na taasisi za Kizayuni na wakaomba serikali ya nchi yao isitishe uhusiano wa kidiplomasia, kibiashara na kijeshi na Israel, ili Chile ijiondoe katika nafasi ya kuwa mshirika asiye wa moja kwa moja wa siasa za kibaguzi za utawala huo.

Mmoja wa wanakamati wa Palestina, akizungumza na waandishi wa habari, alisema: “Chuo kikuu kinapaswa kuwa hifadhi ya fikra za kina na sauti ya haki — si mahali pa kutojali. Ikiwa hata hapa hatuwezi kuzungumza kuhusu haki, basi tutapaza wapi sauti yetu?”

Hatua hiyo ya upinzani ilihitimishwa kwa kaulimbiu isemayo: “Palestina Huru, kutoka Mto hadi Bahari”, na wanafunzi wakatoa ahadi kwamba mikutano ya uhamasishaji na vikao vya mshikamano na watu wa Palestina vitaendelea katika wiki zijazo.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha